Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la Elimu litaweka mwongozo wa elimu duniani hadi 2030- UNESCO

Kongamano la Elimu litaweka mwongozo wa elimu duniani hadi 2030- UNESCO

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, limesema kuwa kongamano la dunia kuhusu Elimu ambalo limefunguliwa leo mjini Incheon, nchini Korea Kusini litaweka mwongozo wa elimu hadi mwaka 2030.

Ajenda ya kimataifa kuhusu elimu kwa kipindi cha miaka 15 ijayo itajadiliwa kwenye kongamano hilo.

Inatarajiwa kuwa azimio kuhusu elimu litaafikiwa kwenye kongamano hilo, likilenga kuchagiza nchi zote na wadau kutekeleza ajenda hiyo mpya, na kupendekeza njia za uratibu, ufadhili na ufuatiliaji wake kwenye ngazi ya kimataifa, kikanda na kitaifa, ili kuhakikisha kuna fursa sawa za elimu kwa wote.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova, ambaye amehutubia kwenye ufunguzi wa kongamano hilo, amesema uwezo wa elimu unajulikana katika kutokomeza umaskini, kubadilisha maisha na kufungua fursa za kutimiza malengo ya maendeleo endelevu. Ameongeza kuwa sote tuna jukumu la pamoja la kumwezesha kila mtoto na kijana kwa misingi inayofaa, mathalan elimu, maadili na stadi, ili kuandaa mustakhbali wao kama raia wenye kuwajibika.