Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana kuhusu hali nchini Somalia

Baraza la Usalama lakutana kuhusu hali nchini Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekutana Jumanne asubuhi kujadili kuhusu hali nchini Somalia, kikao ambacho kimehutubiwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini Somalia, Nicholas Kay, na Mwakilishi wa Kamisheni ya AU na Mkuu wa AMISOM, Maman Sidikou. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Akilihutubia baraza hilo kwa njia ya video kutoka Addis Ababa, Bwana Kay ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM amesema kuwa kwa pamoja, Wasomali wanajenga taifa lao hatua kwa hatua kupitia mazungumzo na maridhiano, licha ya kwamba hali ya kutoaminiana iliyoshamiri kwa zaidi ya miongo miwili inafanya kazi hiyo kuwa ngumu.

Amezungumzia pia hali ya usalama nchini humo, ikiwemo usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na tishio la kundi la kigaidi la Al Shabaab.

“Bado ninatiwa wasiwasi na hali ya usalama Somalia na tishio la Al Shabaab kwenye ukanda mzima, kama ilivyoonyeshwa na shambulizi la kikatili kwenye chuo kikuu cha Garissa nchini Kenya mwezi Aprili. Tunahitaji kufuatilia kwa karibu na kuweza kukabiliana na ishara zozote kuwa Al Shabaab wananufaika kutokana na ushirikiano wao na makundi yenye msimamo mkali Yemen na machafuko huko.”

Mkuu wa AMISOM, Maman Sidikou amesema kuwa hali ya usalama nchini Somalia imetandwa na tishio la ugaidi, kutokana na kuongezeka vitendo vya Al Shabaab, lakini bado AMISOM haitolegeza juhudi zake za kulishinda kundi hilo la kigaidi.