Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Burundi, Janga la kibinadamu lanyemelea Tanzania:WHO

Mzozo Burundi, Janga la kibinadamu lanyemelea Tanzania:WHO

Shirika la afya duniani, WHO limesema janga kubwa la kibinadamu linachipuka Tanzania kutokana na maelfu ya wakimbizi wa Burundi kuendelea kumiminika nchini humo kusaka hifadhi kutokana na mvutano wa kisiasa nchini mwao.

Hofu hiyo inafuatia tathmini iliyofanywa na jopo la wataalamu wa shirika hilo na wale wa Wizara ya Afya nchini Tanzania kuhusu hali halisi mkoani Kigoma na kupendekeza hatua za dharura zichukuliwe.

Mathalani WHO inasema hali inatia shaka zaidi kufuatia kuthibitishwa kwa visa vya Kipindupindu kwenye kambi ya Nyarugusu nchini Tanzania ambako visa vya ugonjwa wa kuhara vilivyoripotiwa ni zaidi ya Elfu Moja.

Halikadhalika WHO inasema kwenye kijiji cha Kagunga nchini humo ambako idadi ya wakimbizi imeongezeka kutoka 11,382 hadi zaidi ya 90,000 tangu kuanza kwa janga hilo mwezi Aprili 2015.

Taarifa ya shirika hilo inasema kuwa makundi yaliyoko hatarini zaidi ni wanawake wajawazito, watoto, wazee na makundi yanayohitaji huduma muhimu zaidi kama vile wanaoishi na virusi vya Ukimwi na wenye ulemavu.