Baraza la Usalama lalaani ghasia mpya zilizoibuka Unity Sudan Kusini

Baraza la Usalama lalaani ghasia mpya zilizoibuka Unity Sudan Kusini

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa wamelaani vikali ghasia mpya ziliyoibuka hivi karibuni kwenye jimbo la Unity nchini Sudan Kusini, kutokana na shambulio la serikali ya Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jumapili hii na Baraza la Usalama, ni zaidi ya watu 100,000 ambao wamelazimika kuhama makwao, aidha shughuli zote za huduma za msingi na za misaada ya kibinadamu zilizokuwa zinasaidia zaidi ya watu 300,000 zimesitishwa kwenye maeneo yaliyoathirika na mapigano.

Halikadhalika, wanachama wa baraza la Usalama wamelaani mashambulizi yaliyofanywa na waasi wa SPLM/A kwenye jimbo la Upper Nile.

Wameeleza wasiwasi wao kuhusu hali ya kibinadamu, watu 50,000 wakiwa wametafuta hifadhi kwenye kambi ya Bentiu ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS na wengine 25,000 kwenye kambi ya Malakal.

Wanachama wa baraza la usalama pia wamelaani vikali ukiukaji wa makubaliano ya sitisho la mapigano baina ya SPLM/A na serikali ya Sudan Kusini ya Januari, 2014 wakisisitiza kwamba hakuna suluhu ya kijeshi kwa mzozo huu unaoendelea tangu miezi 17.