Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wauawa, kutekwa Sudan Kusini: UNICEF

Watoto wauawa, kutekwa Sudan Kusini: UNICEF

Watoto kadhaa wameuawa, takribani 12 kubakwa na wengine kutekwa na kuingizwa jeshini katika mlolongo wa mashambulizi kwenye jimbo la Unity, Sudan Kusini katika kipindi cha wiki mbili kutokana na ushahidi uliopokelewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

Kwa mujibu wa ushahidi huo uliotolewa na watu waliokuwa wanakimbia, vijiji vilivyochomwa moto , watoto wamekuwa wahanga wa machafuko lakini pia wameshiriki machafuko hayo ya karibuni katika jimbo la Unity, wakati wanaume na wavulana waliokuwa na silaha wenye sare rasmi na waliokuwa na nguo za kiraia wakihusika na kufanya uhalifu, wakifanya uharibifu mkubwa na vitu na kukatili maisha ya watu.

Walioshuhudia wanasema wanaamini mshambulizi yametekelezwa na makundi yenye silaha yanayohusiana na Sudan People's Liberation Army (SPLA). Takriban wavulana 19 wengine wakiwa na umri wa miaka 10 na wasichana saba wameuawa na wengine wameingizwa jeshini kwenye mapigano na kuchunga ng’ombe walioibwa.

Inakadiriwa kuwa watoto 13,000 wameingizwa jeshini na wanatumiwa na kila upande katika mapigano kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Umoja wa Mataifa..