Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Djinnit bado yuko Burundi, amezungumza na Rais wa Tume ya Uchaguzi

Djinnit bado yuko Burundi, amezungumza na Rais wa Tume ya Uchaguzi

Mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye ukanda wa maziwa makuu, Said Djinnit bado yuko mji mkuu wa Burundi, Bujumbura kwa lengo la kurejesha utulivu wa kisiasa nchini humo.

Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa Djinnit yuko Bujumbura tangu Ijumaa baada ya kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Tanzania.

(Sauti ya Farhan)

“Ameendelea kuwa na mashauriano na vyama vya siasa, vikundi vya kiraia, mashirika ya kidini, viongozi wa serikali na jamii ya wanadiplomasia kwa lengo la kuanzisha tena mazungumzo ya kisiasa siku zijazo. Halikadhalika leo amekuwa na mazungumzo na Rais wa Tume ya uchaguzi.”

Waandishi wa habari walitaka kufahamu msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhusu uchaguzi nchini Burundi wakati  huu ambapo Muungano wa Afrika unapendekeza uhairishwe kwa sasa..

(Sauti ya Farhan)

“Ni kwamba mashauriano ya Bwana Djinnit yanahusu ni kwa jinsi gani uchaguzi uwe shirikishi na bila ghasia. Iwapo hiyo itahitaji kuahirishwa basi hilo ndilo atapendekeza, lakini kwa sasa  anazungumza na maafisa kutoka pande mbali mbali kuona nini kifanyike.”