Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalam wa UM ataka viwango wastani vya haki kwa walio vizuizini

Mtaalam wa UM ataka viwango wastani vya haki kwa walio vizuizini

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu utesaji, Juan E. Méndez, ametoa wito liridhiwe fungu la sheria kuhusu viwango wastani vya hali ya wafungwa, ambazo zinamulikwa wiki hii na kamisheni kuhusu kuzuia uhalifu na sheria ya uhalifu mjini Vienna.

Sheria hizo zilizofanyiwa marekesbisho zinajumuisha baadhi ya vipengele ambavyo vitawalinda wafungwa zaidi kutokana na utesaji na kutendewa udhalimu mwingine, kama vile kupinga matumizi ya vizuizi vya muda mrefu katika upweke, yaani kwa zaidi ya siku 15.

Bwana Méndez amesema kupitisha na kuetekeleza sheria hizo kutaimarisha kanuni za haki za binadamu na kutoa ulinzi zaidi kwa wafungwa na kutoa mwongozo kwa wasimamizi wa jela.

Sheria hizo zilizofanyiwa marekebisho pia zinajumuisha vipengele muhimu kama vile kutambuliwa kwa kupiga marufuku kabisa utesaji na ukatili mwingine, pamoja na wataalam huru wa afya ambao wanapaswa kujiepusha na kushiriki utesaji huo, wakiwa na jukumu la kutambua na kuripoti dalili za vitendo vya utesaji.