Baada ya jaribio la mapinduzi kushindwa, Burundi epukeni visasi: Kamishna Zeid

Baada ya jaribio la mapinduzi kushindwa, Burundi epukeni visasi: Kamishna Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema kuna hatari kwa Burundi kutumbukia katika zahma kubwa na ametoa wito kwa serikali kuhakikisha watuhumiwa wa jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoshindikana hawakumbwi na visasi,halikadhalika waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu na raia wa kawaida wanaoandamana kupinga serikali .

Zeid amenukuliwa katika taarifa ya ofisi ya haki za binadamu akisema ametoa onyo hilo kufuatia ripoti nyingi wanazopokea kutoka watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari nchini Burundi wakihofia usalama wao.

Amesihi majeshi ya usalama na vikundi vinginenvyo kujiepusha na matukio ya ghasia huku wakipatia kipaumbele usalama wa raia na kuzingatia haki za binadamu wakati huu ambapo vikundi vya kiraia vimetoa wito wa kuanza tena kwa maandamano kwenye mji mkuu Bujumbura.

Kamishna Zeid pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu vitisho vianvyofanywa na wanamgambo wa Imborenakure kwa raia akisema hali hiyo inaweza kusababisah janga kubwa la kibinadamu ambapo tayari zaidi ya raia Laki Moja wamekimbilia nchi jirani.