Usafirishaji haramu wa wahamiaji ni janga lisilopaswa kuendelea- UNODC

Usafirishaji haramu wa wahamiaji ni janga lisilopaswa kuendelea- UNODC

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na dawa na uhalifu, UNODC, Yury Fedotov, amesema kuwa usafirishaji haramu wa wahamiaji ni janga ambalo halipaswi kuachwa likaendelea. Bwana Fedotov amesema hayo katika hotuba yake wakati wa kufungua kikao cha 24 cha kamisheni kuhusu kuzuia uhalifu na sheria ya uhalifu (CCPCJ).

Mkuu huyo wa UNODC ametoa wito wa kuchagiza juhudi za pamoja katika kuimarisha utawala wa sheria na kuzuia aina zote za uhalifu.

Amekumbusha alivyosikitishwa na ripoti za wahamiaji kufariki dunia boti yao ilipozama kwenye Bahari ya Mediterenia mwezi Aprili mwaka huu, wakati wa kongamano la 13 kuhusu uhalifu mjini Doha,

(Sauti ya Yury Fedotov)

“Tangu wakati huo, maelfu ya wahamiaji zaidi na wakimbizi wamefariki kote duniani kwenye safari hatarishi, mara nyingi katika mikono ya makundi halifu ya wasafirishaji haramu. Hatuwezi kuacha hali ii iendelee.”

Ameongeza kuwa usafirishaji haramu wa wahamiaji ni suala linalovuka mipaka na ambalo linaenda moja kwa moja na amani, usalama, haki za binadamu na maendeleo.