Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania : Vifo 7 miongoni mwa wakimbizi wa Burundi

Tanzania : Vifo 7 miongoni mwa wakimbizi wa Burundi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania linachukua hatua za dharura kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa kuhara miongoni mwa wakimbizi wa Burundi waliofika hivi karibuni nchini humo.

Katika taarifa iliyotolewa leo, UNHCR imesema kuwa wakimbizi saba wameshafariki dunia tangu jumatano, wawili wakiwa wamebainishwa na dalili za kipindupindu, thibitisho la maabara likiwa bado linahitajika.

Aidha Warundi 77 kwenye kambi ya Nyarugusu, magharibi mwa mkoa wa Kigoma, na wengine 300 kwenye kijiji cha Kagunga nchini Burundi na Kigoma nchini Tanzania wanatibiwa kwa sababu ya ugonjwa wa kuhara.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania, Joyce Mends-Cole amesema kipaumbele cha shirika hilo ni kushirikiana na wizara ya afya ili kufungua haraka kituo cha kutibu kipindupindu kwenye kijiji cha Kagunga, akieleza kwamba kuna kituo kimoja kidogo tu cha afya kwenye kijiji hicho.

Halikadhalika UNHCR inachukua hatua za kuimarisha usafi na mifumo ya kusafisha maji machafu, pamoja na kuhamisha wakimbizi kutoka Kagunga hadi kigoma na kambi ya Nyarugusu

Kwa mujibu wa mamlaka za serikali ya Tanzania, idadi ya wakimbizi kuoka Burundi imefikia 70,000 nchini Tanzania, 50,000 wakiwa wanaishi kwenye mazingira magumu kwenye kijiji cha Kagunga.