Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wakaribisha makubaliano ya amani nchini Mali

Umoja wa Mataifa wakaribisha makubaliano ya amani nchini Mali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha hatua iliyochukuliwa leo na serikali ya Mali pamoja na baadhi ya waasi ya kusaini makubaliano ya amani na maridhiano.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Ban akisema hii ni hatua muhimu itakayowezesha kufikia amani endelevu na ya kudumu nchini humo, akitumai kwamba utaratibu huu uliofanyika mjini Algiers nchini Algeria utakubaliwa na vikundi vingine vya waasi ambavyo bado vinataka kuendelea na mazungumzo.

Halikadhalika Bwana Ban amekariri wito wake kwa pande zote wa kuheshimu sitisho la mapigano la Mei 2014.

Kwa upande wake Arnauld Akodjenou Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Mali, amekaribisha makubaliano hayo akisema yataruhusu serikali za mitaa kujitegemea zaidi bila kudhoofisha ukamilifu na utawala wa sheria kwa ngazi ya kitaifa.