Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 12 wazaliwa Nepal kila saa bila huduma za msingi

Watoto 12 wazaliwa Nepal kila saa bila huduma za msingi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limekadiria kwamba nchini Nepal, watoto 12 wanazaliwa kila saa wakikosa huduma za msingi za afya, kwa sababu ya kuharibika kwa wodi za uzazi baada ya matetemeko mawili ya ardhi.

Katika taarifa iliyotolewa leo, UNICEF imeonya kuwa maisha ya watoto na wanawake 18,000 yanaweza kuwa hatarini mwezi ujao, iwapo hakuna hatua itakayochukuliwa kukarabati vituo vya afya na hospitali.

UNICEF imeongeza kuwa angalau asilimia 70 ya wodi za uzazi zimeharibiwa katika wilaya 14 zilizoathirika na matetemeko ya ardhi. Aidha nyumba nyingi zimeharibika na wanawake wengi wamekosa sehemu pa kuishi na watoto wao wachanga.

Hata hivyo, hata kabla ya tetemeko la ardhi, asilimia 38 tu ya wanawake kwenye wilaya hizo walikuwa wanajifungua hospitalini.

UNICEF hivi sasa inajitahidi kujenga hospitali za dharura na nyumba za kuhifadhi watoto wachanga na mama zao, pamoja na kusambaza nguo za watoto, vitamini na vifaa vya kuzalisha watoto kwenye maeneo yaliyoathirika.