Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisho la mapigano halitoshi kufikia watu wote nchini Yemen: OCHA

Sitisho la mapigano halitoshi kufikia watu wote nchini Yemen: OCHA

Nchini Yemen, wakati sitisho la mapigano la siku tano lililoanza jumanne likiendelea, mkuu wa ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA nchini humo, Johannes Van der Klauw amesema bado baadhi ya watu hawajafikiwa kwa sababu mapigano yanaendelea kwenye maweneo kadhaa.

Hata hivyo Bwana Van Der Klauw amesema sitisho la mapigano limewezesha watu kupata nafuu.

(SAUTI VAN DER KLAUW)

“ Lengo la sitisho hilo ni kuwaruhusu watu kukimbia maeneo ya mapigano, kupata nafasi ya kupumua na kupewa huduma za msingi. Inaturuhusu pia kuondoa maiti, na kuwapeleka wajeruhi ili wapate matibabu ya awali” 

Aidha mkuu wa OCHA ameeleza kuwa ukosefu wa mafuta ni tatizo kubwa nchini humo.

(SAUTI VAN DER KLAUW)

“Kama mafuta ya ziada hayapatikani katika wiki chache zijazo, hospitali zitafungwa, mifumo ya maji na kusafisha maji machafu itasitishwa, huduma za simu zitaisha na umeme utakatika nchini kote kwa sababu hakuna umeme, kila kitu kinafanya kazi kwa jenerata, ambazo zinahitaji mafuta”

Kwa mujibu wa OCHA, idadi ya wakimbizi wa ndani imefikia 450,000.