UNESCO yataka eneo la urithi Palmyra lilindwe
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO), Irina Bokova amelezea kusikitishwa na taifa za mapigano karibu na eneo la kihistoria liitwalo Palmyra nchini Syria amabayo amesema yanahatarisha jamii ya eneo hilo na uwepo wa eneo hili ambalo liko katika orodha ya maeneo ya urithi ya UNESCO.
Ametaka kusitishwa kwa mapigano mara moja, ambapo vyanzo vinadokeza kuwa makundi yenye msimamo mkali yamevamia mji wa Tadmur ambalo ndiko liliko eneo hilo la kihistoria la Palmyra linaloelezwa kuwa eneo muhimu zaidi la utamaduni huko Mashariki ya Kati.
Palmyra inawakilisha masalio ya kipekee ya karne ya kwanza na usanifu wa miji ya Kirumi pamoja na kumbi maarufu katika mtaa mkuu na hekalu la Baal ambayo ni utamaduni muhimu katika ukanda huo.
Mkuu huyo wa UNESCO amesema kuwa eneo hilo limeshuhudia mateso kwa miaka minne sasa wa uporaji, jambo linaloonyesha kuwa hakuna hazina mbadala kwa watu wa Syria na dunia.
Bi Bokova ametaka pande kinzani kulinda Palmyra na kufanya kila wawezalo kulinda uharibifu .