UNAIDS yahimiza mshikamano kutetea wapenzi wa jinsia moja

UNAIDS yahimiza mshikamano kutetea wapenzi wa jinsia moja

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Ukimwi, UNAIDS, Michel Sidibé ametoa wito kwa kila mmoja kujiunga kwenye vuguvugu linalopigania haki ya kijamii na usawa ili kila mtu aishi katika utu na heshima. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Bwana Sidibé amesema hayo leo, ikiwa ni siku chache kabla ya maadhimisho ya siku ya kupinga chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia, mnamo Jumamosi tarehe 17 Mei.

Amesema ulimwengu wa sasa unashuhudia mabadiliko ya kijamii kwa kasi, huku wapenzi wa jinsia moja, wale wanaopenda watu wa jinsia zote na wale wanaojitambulisha kwa jinsia mbili wakiwa wamepiga hatua kubwa katika kupigania haki zao. Licha ya ufanisi huu, amesema bado kuna vitendo vya ubaguzi na ukatili dhidi ya watu hao, na hivyo kuhimiza mshikamano wa kimataifa katika kutetea haki zao.

Ameongeza kuwa jamii ya sasa haiwezi kuvumilia vitendo vya kuchagua haki za binadamu, kwani ni jamii inayosherehekea utofauti, na kwamba kila mtu anastahili kuishi kwa amani na usalama na kuchangia jamii yake bila kujali anaishi wapi au anampenda nani.