Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yahaha kunusuru wakulima Sudan Kusini

FAO yahaha kunusuru wakulima Sudan Kusini

Msimu wa upanzi ukiwa unaanza nchini Sudan Kusini, shirika la kilimo na chakula FAO linajitahidi kupata mbegu muhimu, vifaa na malighafi nyingine kwa ajili ya baaadhi ya wakulima walio katika mazingira hatarishi kufuatia machafuko.

Katika kufanikisha hili ndege 18 za FAO  zikiwa na mbegu na vifaa kazi ikiwamo vya kuvulia huondoka Juba kila siku lengo likiwa kuwafikia wakulima kwa wakati hususani ni katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano jimboni Upper Nile na Jonglei ambapo kiwango cha njaa na utapiamlo ni kikubwa. Taykribani tani 1000 zimeagizwa kuzifikia zaidi ya familia 175, 000 ambazo hazina chakula  kabla ya mwisho wa mwezi May.

Dominique Burgeon ni mkuu wa kitengo cha dharura cha FAO

(SAUTI DOMINIQUE)

Tunalenga kuwafikia takribani watu milioni mbili na laki nane, wengi wao tayari wameshapokea vifaa vya kilimo ikiwamo mbegu za mazao, mbogamboga, na vifaa vya uvuvi. Hii ndio fursa pekee kwa mwaka huu, wakishindwa kuandaa mashamba sasa, hali zao zitadorora zaidi.’

Shirika  hilo la chakula na kilimo linasema kuwa kufuatia  miundo mbinu mibovu maeneo hayo hayafikiki kwa barabara.