Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 1,000 huambukizwa Kipindupindu kila wiki nchini Haiti

Watu 1,000 huambukizwa Kipindupindu kila wiki nchini Haiti

Mratibu wa Umoja wa Mataifa kwa maswala ya kipindupindu nchini Haiti, Pedro Medrano Rojas, amesema ni lazima kutosahau janga la kipindupindu nchini Haiti, akiongeza kwamba bado ni swala la dharura nchini humo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani WHO, tayari watu 113 wamefariki dunia tangu mwanzo wa mwaka huu nchini Haiti ambako watu 1,000 huambukizwa kila wiki.

Bwana Medrano Rojas ameeleza kwamba ongezeko la visa vipya mwaka huu limesababishwa na mvua nyingi za mwezi Septemba mwaka jana na hasa upungufu wa ufadhili, tayari vituo 91 miongoni mwa vituo 250 vilivyopo nchini humo vimefungwa.

Amesema cha kusikitisha ni kwamba ugonjwa huu unatibiwa, na kinachohitajika tu ni ufadhili ili kuwapatia watu matibabu.

Tangu kulipuka kwa kipindupindu nchini Haiti mwaka 2010 watu 9,000 wamefariki dunia, huku 735,000 wakiambukizwa ugonjwa huo.