Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utafiti mpya waonyesha athari za njaa kwa uchumi wa Malawi

Utafiti mpya waonyesha athari za njaa kwa uchumi wa Malawi

Uchumi wa Malawi hupoteza takriban dola milioni 600 kila mwaka kutokana na athari za lishe duni miongoni mwa watoto, imesema ripoti mpya iliyozinduliwa leo mjini Lilongwe. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Ripoti hiyo iitwayo, gharama ya njaa barani Afrika, inamulika athari za kijamii na kiuchumi zitokanazo na lishe duni miongoni mwa watoto nchini Malawi.

Ripoti hiyo ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, inaonyesha kuwa taifa hilo hupoteza kiasi kikubwa cha fedha kila mwaka kutokana na lishe duni miongoni mwa watoto, ambayo huchangia kuongezeka gharama ya matibabu, mzigo wa ziada kwa mfumo wa elimu na uzalishaji mdogo miongoni mwa wafanyakazi. Elisabeth Byrs ni msemaji wa WFP

Nchini Malawi, watoto wapatao miliioni 1.4 wamedumaa. Hii inamaanisha wakiwa watu wazima, hawawezi kufanya kazi vizuri, au wanaumwa mara kwa mara, au watoto wanaoacha shule mapema au hawaendi shule, na hatimaye, mchango wao kikazi haulingani na ule wa watu wenye nguvu kamili.”

WFP imependekeza taifa hilo liweke malengo ya kupunguza kudumaa kwa asilimia 23 ifikapo mwaka 2025.