Skip to main content

Kisa cha Ebola chathibitishwa Italia: WHO

Kisa cha Ebola chathibitishwa Italia: WHO

Mgonjwa mmoja wa Ebola amethibitishwa huko Italia, na hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ambazo Shirika la afya duniani WHO limepokea kutoka nchini humo kikiwa ni kisa cha kwanza.

WHO inasema mgonjwa huyo ni mhudumu wa afya ambaye amerejea kutoka Sierra Leone ambako alikuwa anatoa huduma katika kituo cha matibabu ya Ebola nchini humo.

Mgonjwa huyo alirejea tarehe Saba mwezi huu kutokea Freetown akipitia Casablanca, Morocco.

Hata hivyo WHO imesema hakuwa na dalili zozote za Ebola alipowasili mjini Roma, Italia lakini saa 72 ndipo dalili zilikuwa dhahiri.

Kwa sasa mgonjwa huyo anaendelea na matibabu chini ya uangalizi mkubwa ili kuepusha maambukizi ambapo WHO imesema itaendelea kutoa taarifa kupitia mfumo wake wa utoaji taarifa kuhusu harakati dhidi ya Ebola.