Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yazitaka Indonesia na Malaysia ziwapokee walio hatarini

UNHCR yazitaka Indonesia na Malaysia ziwapokee walio hatarini

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNCHR, limeeleza kusikitishwa na ripoti kwamba huenda Indonesia na Malaysia zilizifukuza boti zilizowabeba watu walio hatarini kutoka Myanmar na Bangladesh.

Mnamo Jumatatu, jeshi la wanamaji la Indonesia lilisema kuwa lilikuwa limeisindikiza boti moja kurudi baharini, huku mamlaka ya bahari ya Malaysia ikitangaza kuwa haitoruhusu meli za kigeni kutia nanga, ila tu pale zinapokuwa zimeharibika au zinazama.

UNHCR imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kunusuru maisha, wakati watu zaidi wakilazimika kutafuta hifadhi nje ya mipaka ya nchi zao kufuatia migogoro na udhalimu katika nchi zao.

Volker Türk, Msaidizi wa Kamishna Mkuu wa UNHCR kuhusu ulinzi wa wakimbizi, amesema la kipaumbele ni kuokoa maisha, akiongeza kuwa badala ya kukwepa kuwajibika, serikali zinapaswa kugawana majukumu ya kuwasaidia watu hao mara moja.