Mkuu wa OCHA atolea wito sitisho la mapigano Yemen
Nakaribisha kuanza kwa sitisho la mapigano huko Yemen linalolenga kupisha mashirika ya misaada ya kibinadamu na wadau wao kuwafikia wahitaji, amesema Mratibu Mkuu wa usaidizi wa kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa Valerie Amos.
Bi. Amos ametoa kauli hiyo kufuatia uamuzi wa pande kinzani huko Yemen kuridhia siku tano za kusitisha mapigano ili misaada hiyo ya kimsingi iweze kufikia wahitaji.
Ametoa wito kwa pande hizo kuheshimu hatua hiyo akisema itatoa fursa kwa raia walionaswa kwenye eneo la mapigano kwani watapatiwa misaada ya chakula na dawa muhimu kuwafikia
Bi. Amos ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya misaada ya kibinadamu, OCHA ametoa shukrani zake kwa nchi wanachama kwa kusaidia juhudi za kuwezesha mashirika ya misaada kufikia wananchi.
Amesema kwa kuzingatia kuwa mashirika hayo hayaegemei upande wowote ni vyema yakatoa usaidizi wake kupitia mifumo ya Umoja wa Mataifa ili kuepusha misaada hiyo kupatiwa mtazamo wa kisiasa.