Bosnia na Herzegovina yastahili kuona matumaini miaka 20 baada ya vita: Baraza
Jamii ya kimataifa inapaswa kuisaidia Bosnia na Herzegovina kupata uwezo wa kujitegemea, amesema mwakilishi mkuu nchini humo Valentin Inzko wakati alipohutubia Baraza la Usalama lilipokutana leo juu ya hali iliyopo nchini humo.
Kwenye mkutano huo unaofanyika kila baada ya miezi sita, Bwana Inzko amesema mafanikio mengi yamepatikana tangu makubaliano ya amani ya Dayton ya mwaka 1995, lakini bado chamgamoto ni nyingi.
Ameeleza kwamba, baadhi ya wanasiasa wanajaribu kurudisha nchi nyuma na kuchochea chuki za kikabila, lakini licha ya hayo watu wengi zaidi nchini Bosnia na Herzegovina wameanza kuwa na mtazamo mpya wa kuangalia mbele, wakisaidiwa na juhudi za Muungano wa Ulaya.
“ Ni sawa kabisa kwamba baada ya miaka 20, raia wa Bosnia na Herzegovina, hasa vijana, wanategemea mengi zaidi kutoka kwa nchi yao na wanasiasa wao. Wanakumbwa na uwiano wa ukosefu wa ajira mkubwa zaidi barani Ulaya na wengi wanakimbia nchi. Wana haki ya kutarajia zaidi kwa sababu kweli Bosnia na Herzegovina ina uwezo wa kuwanufaisha raia wake na kuwapatia maisha ya kawaida”