Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yasikitishwa kuzuka kwa mapigano Darfur

OCHA yasikitishwa kuzuka kwa mapigano Darfur

Kaimu mratibu mkazi wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA nchini Sudan, Geert Cappalaere ameelezea kusikitishwa kwake na taarifa za kuzuka kwa mapigano ya makabila kwenye jimbo la Darfur Mashariki.Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte

(TAARIFA YA PRISCILLA)

Taarifa ya OCHA inamnukuu Bwana Cappalaere akisema kuwa mapigano hayo yamezuka katika miji iitwayo Abu Karinka na Adila na kueleza kuwa wengi wa wakazi katika miji hii ni wanawake na watoto wasio na hatia na wasiopaswa kubeba mzigo wa mapigano mapya.

Amezikumbusha pande kinzani kuwa zina wajibu wa kulinda raia na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia walengwa huku akizitaka pande hizo kusitisha mapigano mara moja kwa kujizuia pamoja na kuunga mkono juhudi za upatanishi kwa njia ya amani.

Zaidi ya raia 120000 katika eneo hili walipotea makazi kutokana machafuko ya kikabila yaliyozuka mwaka 2013.