Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tetemeko lingine laikumba Nepal:UNICEF

Tetemeko lingine laikumba Nepal:UNICEF

Tetemeko lingine lenye ukubwa wa 7.4 vipimo vya rishter limeikumba Nepal. Tetemeko la leo  lililotikisa zaidi Kathmandu linafuatia lile la Aprili 25 lililokatili maisha ya watu zaidi ya 8000 na kujeruhi wengine wengi huku likiharibu miundombinu, na nyumba za watu. Taarifa ya Amina Hassan inafafanua zaidi.

(TAARIFA YA AMINA HASSAN)

Mmoja wa wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF amesema wakati tetemeko la leo likitokea ilibidi wajifiche chini ya meza wakati jengo la ofisi yao likitikiswa kutoka upande mmoja kwenda mwingine huku wakijihisi wako ndani ya boti inayoyumbishwa na mawimbi makali.

Ingawa walifanikiwa kutoka salama baada ya hali kutumia lakini wafanyakazi wote wanalolifikiria ni athari ya tetemeko la leo kwa mamilioni ya watoto ambao tayari wamepitia makubwa kutokana na tetemeko la kwanza la Aprili.

UNICEF inasema watoto milioni 1.7 wanahitaji haraka msaada wa kibinadamu ikiwemo maji salama ya kunywa, vifaa vya usafi, madawa na ushauri nasaha, na shirika hilo limesema litafanya kila liwezekanalo kuhakikisha watoto wako salama. Rupa Joshi ni mfanyakazi wa UNICEF Nepal

(CLIP YA RUPA JOSHI)

"Kuna eneo kubwa la wazi  katikati ya mji ambako tayari watu walishaanza kuondoka wiki jana  akini  nadhani kutakuwa na watu wengi waliopoteza makazi yao hapo leo. Walikuwa tayari wanasahau hofu kutokana na tetemeko la kwanza. Na  watu  walioko vijijini ambao nyumba zao zilikuwa zimeharibika kabisa na ardhi ilikuwa inatetemeka na maporomoko ya udongo. Pia jinsi hii itaathiri watoto ambao tayari walikuwa na kiwewe. Hilo  ndilo linasikitisha."