Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la Ebola limefichua udhaifu dhidi ya magonjwa:Ripoti

Janga la Ebola limefichua udhaifu dhidi ya magonjwa:Ripoti

Sasa ni wakati wa kihistoria kwa viongozi wa dunia kuonyesha utashi wao wa kisiasa kuwezesha shirika la afya duniani, WHO kuongoza harakati za afya duniani.

Hiyo ni moja ya mapendekezo ya  awali ya ripoti ya jopo huru la wataalamu lililoundwa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO kuchunguza hatua zilizochukuliwa na shirika hilo kukabiliana na Ebola.

Pendekezo hilo limezingatia vikwazo viliyobainika kukwamisha juhudi za WHO dhidi ya Ebola ambavyo ni pamoja na ukata, ukosefu wa watendaji na kanuni za kimataifa za afya.

Ripoti hiyo  imewekwa bayana leo huko Geneva na mchunguzi mkuu Barbara Stocking, ambaye ametolea mfano jinsi miongozo ya kudhibiti Ebola ilivyokuwa inakanganya umma.

 (Sauti  ya Barbara)

“Sasa imefahamika bayana, baadhi ya baadhi ya ujumbe wa kuhamasisha umma ulikuwa mkali sana ukisema ‘Ebola inaua’. Sasa kama Ebola inaua na hauna la kufanya kwa nini basi mgonjwa aende kituo cha afya? Tunafahamu mwanzoni watu walisema watu wanaokuja kuwatibu wanakuja na virusi vya Ebola. Kwa hiyo wakati huo mambo yote hayo yalikuwa yanaendelea. Hatudhani iwapo ushirikishi wa jamii ulifanyika kwa umakini.”

Ripoti hiyo ya kurasa 12 inapendekeza mabadiliko ili WHO iweze kukabili ipasavyo dharura kama Ebola lakini akasema WHO pekee haiwezi bila kuungwa mkono na nchi wanachama..

(Sauti ya Barbara)

“Ni lazima kuwepo na uwajibikaji wa hili unafahamu WHO ni lazima itoe mpango wake wa mabadiliko, lakini hiyo inahitaji nchi wanachama kuchangia angalau fedha. La sivyo  haiwezi kufanyika lazima nchi wanachama ziunge mkono na hilo ndilo muhimu.”

Ripoti hiyo imesema hakuna sababu ya kuunda chombo kingine bali WHO kwani shirika hilo lina wataalamu wa kutosha  badala yake kuwe na kitengo ndani  yake chenye uwezo thabiti wa kuhusika na dharura za magonjwa.