Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la Mediteranea lahitaji mshikamano dunia nzima:EU

Janga la Mediteranea lahitaji mshikamano dunia nzima:EU

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kilichoangazia ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na taasisi za kikanda kwa lengo la kuendeleza amani na usalama duniani hususan janga la wahamiaji Mediteranea. Taarifa zaidi na Flora Nducha.

(Taarifa ya Flora)

Federica Mogherini, Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Muungano wa Ulaya kuhusu masuala ya kigeni na usalama alikuwa wa kwanza kuhutubia akiangazia janga linalokumba wahamiaji wanaokimbia Afrika na Mashariki ya Kati kusaka usalama na maisha bora barani Ulaya.

Hapa anasema mwaka 2015 hali ilikuwa mbaya kwa wasaka hifadhi kuliko miaka iliyotangulia na wito wake ni mshikamano siyo tu kutoka nchi ambako wahamiaji wanakwenda bali pia wanakotoka akisema kuwa wakati mwingine maeneo ya mpito yanageuka kuwa makazi ya kudumu, hivyo akasema..

(Sauti ya Federica-1)

“Twahitaji ubia iwapo tunataka kumaliza janga hili. Tunapaswa kufikiri na kuchukua hatua pamoja. Twahitaji uwabijikaji wa pamoja. Ni wajibu wa Ulaya na dunia nzima.”

Akatoa hakikisho..

(Sauti ya Federica-2)

“Nitoe hakikisho bayana, hakuna mhamiaji au mkimbizi atakayekutwa baharini atarejeshwa kwao bila ridhaa yake. Haki zao kwa mujibu wa mkataba wa Geneva zitazingatiwa.”

Mwakilishi wa Muungano wa Afrika barani Ulaya Balozi Tete Antonio akasema Libya ni kiini na njia ya mpito kwa wahamiaji hivyo..

(Sauti ya Tete)

 “Jaribio lolote la kushughulikia suala hilo ni lazima lishughulikie mzozo wa Libya.”