Skip to main content

Mtaalamu wa haki za binadamu kuzuru Sudan baada ya muongo mmoja

Mtaalamu wa haki za binadamu kuzuru Sudan baada ya muongo mmoja

Mwakilishi maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Rashida Manjoo atazuru Sudan tarehe 13 hadi 24 Mai mwaka huu ili kutathmini kwa ujumla hali ya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, na kukusanya taarifa kutoka kwa wahanga wa ukatili huo.

Bi Manjoo amesema atakutana na wanaharakati wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake kuangalia hali katika maeneo ya vita na yasiyo na vita, ukiwemo ukatili dhidi ya wanwake wakimbizi na wakimbizi wa ndani.

Hii ni ziara ya kwanza ya mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kwenda Sudan tangu mwaka 2005, ya kutathimini hali, kutoa ripoti na ushauri kuhusu hali ya ukatili dhidi ya wanawake kote duniani.

Wakati wa ziara yake hiyo ya siku 13 pia Bi Manjoo atakutana na viongozi wa serikali, jumuiya za kijamii, wanaharakati wengine mjini Khartoum, jimbo la Darfur, ikiwemo maeneo ya El Fasher, Thabit, El Geneina na Nyala, pamoja na jimbo la Kordofan. Kaskazini na Kusini.