Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili kuhusu vurugu Burundi

Baraza la Usalama lajadili kuhusu vurugu Burundi

Baraza la Usalama leo limekutana katika kikao cha faragha kujadili kuhusu Burundi, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Said Djinnit akiwaelezea wanachama wa baraza hilo kwa njia ya video kutoka Bujumbura jitihada alizozifanya ili kutafuta suluhu ya kisiasa kwa mzozo huu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu, Mwakilishi wa Kudumu wa Lithuania Raimonda Murmokaite ameelezea wasiwasi wa baraza hilo kuhusu hali iliyopo nchini humo na kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi kwenye nchi jirani.

Aidha amesema wanachama wa baraza la usalama wameziomba pande zote nchini Burundi kujizuia na kutumia ghasia na wamezingatia umuhimu wa kuwa na utaratibu wa uchaguzi wenye uhuru na uwazi, pamoja na uhuru wa kujieleza.

Balozi Murmokaite ameongeza kwamba wanachama wa baraza hilo wamekaribisha juhudi za Muungano wa Afrika, AU, za Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC na za IGAD.

« Wanachama wa baraza la usalama pia wamekariri utayari wao wa kuendelea kufuatilia kinachoendelea nchini Burundi hadi hali ya kisiasa na kiusalama itaimarika na pande zote zikubali kutunza amani na utulivu Burundi, na pia kuchukua hatua dhidi ya kitendo chochote kitakachohatarisha amani na usalama nchini humo, ikiwemo kuchochea ghasia na kusambaza silaha »

Kwa upande wake mwakilishi wa kudumu wa Marekani Samantha Powers amesikitishwa na uamuzi wa rais Pierre Nkurunziza akisema Burundi sasa inaathirika na matokeo ya uamuzi huo.