Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yafungua kambi mpya Iraq

IOM yafungua kambi mpya Iraq

Shirika la Uhamiaji duniani IOM limefanikiwa kujenga kambi mpya ya wakimbizi wa ndani nchini Iraq kwa ushirikiano na mashirika mengine ya kimataifa. Tayari familia 500 zimehamia kwenye kambi hii ya Shekhan iliyopo kaskazini mwa Iraq na mamia wengine wanatarajiwa  kuhamia kambini kwenye siku zijazo.

Kwa jumla kambi ya Shekhan ina uwezo wa kuzipatia hifadhi familia 1,000. Ujenzi wa kambi hiyo umefadhiliwa na Saudi Arabia na itaongozwa na serikali ya wilaya ya Dohuk.

Tayari kambi 16 zimejengwa kwenye wilaya ya Dohuk ambapo wakimbizi wa ndani 450,000 wametafuta hifadhi kutoka maeneo jirani ya Sinjar lakini asilimia 38 ya wakimbizi hawa bado wanaishi kwenye majengo duni.

Kwa mujibu wa IOM, idadi ya wakimbizi wa ndani nchini Iraq kwa jumla imefikia zaidi ya milioni 2.6.