Walinda amani wa Tanzania nchini DRC washambuliwa

Walinda amani wa Tanzania nchini DRC washambuliwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali mashambulizi yaliyotokea jumanne hii dhidi ya walinda amani wa Tanzania waliopo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na kusababisha vifo vya walinda amani wawili na kujeruhi 13. Taarifa zaidi na Grace Kaneyia

(TAARIFA YA GRACE KANEIYA)

Mashambulizi hayo yametokea kwenye maeneo ya Beni, kaskazini mwa DRC, wakati kundi la waasi wanaoshukiwa kuwa ADF lilivamia msafara wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO.

Tukio hili linafuata shambulio jingine lililotokea jumatatu wakati helikopta ya MONUSCO iliyokuwa inasafirisha kamanda mkuu wa MONUSCO ililazimishwa kutua kwa haraka baada ya kupigwa risasi.

Akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa kamanda huyo Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz amesema hali hii haiwezi tena kukubaliwa.

(CLIP YA DOS SANTOS CRUZ)

Ni lazima kuchukua hatua ya nguvu sana ili kubatilisha na kutokomeza maharamia hawa. Nadhani ADF ni kundi la magaidi. Tutawasaka na kutumia njia zote ili kuwabatilisha na kuwatokomeza ikiwa ni lazima »

Katibu Mkuu amepeleka salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa MONUSCO Martin Kobler ambaye leo amewatembelea majeruhi amesema mashambulizi hayo yanaonyesha umuhimu wa kurejesha ushirikiano kati ya MONUSCO na jeshi la DRC kwa ajili ya usalama wa eneo hilo.