Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya umaskini, Chad na Niger ziko mstari wa mbele kukaribisha wakimbizi

Licha ya umaskini, Chad na Niger ziko mstari wa mbele kukaribisha wakimbizi

Mkurugenzi wa operesheni za ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, John Ging amesema licha ya kuwa kwenye nchi maskini zaidi duniani, raia wa Chad na Niger ni watu wakarimu ambao hawakusita kupokea wakimbizi kutoka nchi jirani kama vile Nigeria.

Kiongozi huyo wa OCHA amesema hayo akizungumza leo na waandishi wa habari mjini New York. Ameeleza kwamba nchi za Niger na Chad ambazo ni za mwisho kwenye orodha ya maendeleo zinapaswa kuwa za kwanza kwenye ajenda ya usaidizi wa Umoja wa Mataifa.

Bwana Ging ambaye alikuwa ziarani Chad na Niger siku chache zilizopita, amesema jamii ya kimataifa inapaswa kuongeza bidii ili kufadhili operesheni za misaada ya kibinadamu kwenye nchi hizo, akieleza kwamba nchi hizo mbili zimepokea wakimbizi 700,000, wakati tayari asilimia 25 ya raia wa nchi hizo wanategemea misaada ya kibinadamu.

(SAUTI GING)

“ Mtu akihusiana na raia kwenye maeneo hayo, anapaswa kuwapa changamotio vongozi wa kisiasa ili wawe karibu zaidi na raia wa kawaida. Swala si tu la utulivu wao, si utulivu wa kikanda tu, bali pia utulivu wa dunia nzima. Kwa hiyo tunapaswa kubadilisha msimamo wetu ili tujitahidi zaidi na kwa njia bora kwa ajili ya hawa watu wazuri. »

Wito wa ufadhili kwa ajili ya Niger na Chad umetimizwa kwa takriban asilimia 20 pekee.