Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Sudan pengine sababu ya mlipuko wa Surua:UNICEF

Mzozo Sudan pengine sababu ya mlipuko wa Surua:UNICEF

Kuendelea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Surua huko Sudan kumesababisha Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kufikiwa kwa watoot 500,000 na familia zao walio kwenye maeneo yasiyofikika kwa miaka minne sasa kutokana na mizozo.

Majimbo 14 kati ya 18 nchini huyo tayari yamekumbwa na Surua ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema hadi sasa visa 2,200 vya ugonjwa huo vimethibitika nchini humo.

UNICEF inasema idadi hiyo ya visa ni mara nne zaidi ya wastani wa wagonjwa katika kipindi cha miaka miwili iliyotangulia na nusu yao ni watoto walio na umri wa chini  ya miaka mitano.

Vifo vingi kutokana na Surua vinaripotiwa zaidi Darfur Mashariki ambako watoto 27 hadi sasa wamefariki dunia.

Geert Cappelacre ni mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan.

(Sauti ya Geert)

Kwa sababu ya mzozo kwenye maeneo hayo tumeshindwa kufikia jamii kwa kipindi cha miaka minne iliyopita. Kwa hiyo tuna idadi kubwa ya watoto huko ambao hawajapatiwa chanjo na hiyo inaweza kuwa moja ya sababu ya mlipuko wa Surua tunaoshuhudia sasa.”

UNICEF inataka deni la nje la Sudan ambalo ni dola Bilioni 46 zilitathminiwe upya ili nchi hiyo iweze kuwekeza kwenye afya, lishe na elimu.