Makundi yenye silaha CAR yakubali kuachilia maelfu ya watoto:UNICEF
Viongozi wa makundi yenye silaha nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, leo Jumanne wamekubali kuachilia watoto wote wanaohusishwa na majeshi yao na kumaliza mara moja uingizaji mpya wa watoto jeshini. Taarifa ya Grace Kaneiya inafafanua.
(TAARIFA YA GRACE KANEIYA)
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataoifa la kuhudumia watoto UNICEF takribani watoto 6000 hadi 10,000 wanahusishwa hivi sasa na makundi yenye silaha nchini CAR. Idadi hiyo inajumuisha wale wanaotumiwa kama wanajeshi , wanotumiwa kwa ngono na wale wanaofanyishwa kazi za upishi, wajumbe na shughuli zingine.
UNICEF inasema hii ni hatua kubwa katika kuwalinda watoto nchini humo. Jamhuri ya Afrika ya Kati ni moja ya mahali pabaya zaidi duniani kuwa mtoto, na UNICEF iko tayari kufanyakazi na uongozi ili kusaidia kuwaunganisha tena watoto hao na familia zao. Kama anavyofafanua msemaji wa shirika hilo Christophe Boulierac.
(SAUTI YA CHRISTOPHE BOULIERAC)
"Tunafanya kazi na jamii na viongozi wa kijamii kuhakikisha kwamba watoto hawa hawanyanyapaliwi, hicho ndicho kipaumbele kuhakikisha kwamba wanakubaliwa na jamii ambako tunataka warudi na ambako familia wanataka warudi."
Makubaliano ya kuachiliwa kwa watoto hao yaliyofanikishwa na UNICEF na washirika wake yalitiwa saini wakati wa wiki nzima ya kongamano la maridhiano ya kitaifa linaloendelea mjini Bangui tangu Mai 4 hadi Mai 11kwa lengo la kurejesha amani katika taifa hilo lililoghubikwa na machafuko.