Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM inawasaidia wahamiaji wa Chad waliokwama Cameroon kurejea nyumbani

IOM inawasaidia wahamiaji wa Chad waliokwama Cameroon kurejea nyumbani

Ikiwa ni miaka mitatu tangu kuzuka kwa machafuko nchini Jamhuri ya Kati CAR, shirika la kimataifa la uhamiaji IOM linaendelea kuwasaidia wahamiaji wa Chad waliokwama nchini Cameroon baada ya kukimbia vita CAR na sasa wanataka kurejea nyumbani.

Mwishoni mwa wiki IOM ilisafirisha wahamiaji wa Chad 179 kutoka Cameroon hadi Chad kwa njia ya barabara. Wahamiaji hao walikuwa wanahifadhiwa kwenye eneo la muda la Djako Kusini mwa Chad.

Eneo hilo linasimamiwa na IOM huku mashirika mengine kama la mpango wa chakula duniani WFP likigawa chakula, la kuhudumia watoto UNICEF likitoa huduma ya maji na vifaa vya usafi na kamati ya kimataifa ya uokozi ICRC inatoa huduma za afya.

Kufuatia machafuko ya CAR yaliyozuka Disemba 2013 maelfu ya wahamiaji wamelazimika kukimbia kuokoa maisha yao ama kwa kurejea nchini mwao au kwa kutafuta hifadhi ya ukimbizi nchi jirani zikiwemo Chad, Cameroon, Niger na Congo Brazzaville.