Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mustakhbali wa Syria waangaziwa Geneva:

Mustakhbali wa Syria waangaziwa Geneva:

Mashauriano kuhusu mustakhbali wa Syria yameanza huko Geneva, Uswisi ambapo mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura ameweka bayana kuwa mkusanyiko huo siyo awamu ya tatu ya mkutano wa kimataifa kuhusu Syria.

Akizungumza na waandishi wa habari Bwana de Mistura amesema badala yake kusanyiko hilo la aina yake linalotarajiwa kwa kuanzia kudumu kwa wiki tano, litakuwa la mashauriano na majadiliano ya faragha ya kina yakilenga kusaka hitimisho la mzozo wa Syria ulioingia mwaka wa tano huku juhudi hata za kusitisha mapigano zikigonga mwamba.

(Sauti ya de Mistura)

 "Kwa hiyo tunaanza mlolongo wa majadiliano na kila upande mmoja mmoja kutoka pande zote zinazohusika na mzozo wa Syria ili kuweza kupata taswira halisi iwapo awamu nyingine ya mashauriano itawezekana hapo baadaye na Syria ya baadaye yenye amani itakuwa namna gani. Msitarajie tangazo lolote kwa umma wakati au mwishoni mwa mchakato huu. Nitaripoti kwa katibu mkuu.”

Kwa mujibu wa mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, zaidi ya vikundi 40, bila shaka serikali ya Syria, taasisi, watu binafsi na wawakilishi 20 wa kikanda na kimataifa, nchi jirani na wajumbe watano wa kudumu wa baraza la usalama wanashiriki mashauriano hayo, na wigo wa ujumbe unaweza kuongezeka iwapo itaonekana ni muhimu kufanya hivyo.