Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi 1,000 kutoka DRC wapokelewa Uganda

Wakimbizi 1,000 kutoka DRC wapokelewa Uganda

Zaidi ya wakimbizi Elfu Moja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wamepokelewa nchini Uganda katika wiki mbili zilizopita, kufuatia kuibuka upya kwa ukatili unaofanywa na vikundi vilivyojihami mashariki mwa nchi hiyo. John Kibego na maelezo zaidi kutoka Uganda.

(Taarifa ya John Kibego)

Wote wamesajiliwa kwenye kituo cha kupokea wakimbizi cha Nyakabande wilayani Kisoro. Wameingia kupitia mipaka ya Nyabwishenya na Bunanaga katika wilaya hiyo, na wengine kwenye mpaka wa Ishasha katika wilaya jirani ya Kanungu.

Wanadai kukimbia ongezeko la vitendo vya ubakaji na kulazimishwa kijiunga na wanamgambo wa Mai katika katika Mkoa wa Kivu ya Kaskazini, ambao wanaarifiwa kuwa wanajiimarisha upya, baada ya kuvunjwa nguvu na jeshi la serikali ya nchi hiyo mwaka jana.

Pauline Abina kamandanti wa kambi ya Nyakabande amesema, katika ushirikiano na Shirika la Umoja wa Matifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) wameanza kuwahamisha hadi kwenye kambi ya Rwamwanje.

(Sauti ya Pauline Abina)

“Kufikia jana tulikuwa na wakimbizi 1168. Kisha tulihamisha wakimbizi 544 hadi kwenye kambi ya Rwamwanje wilayani Kamwenge na huko ndiko tuakowapeleka wote tunaowapokea hapa”

Uganda inahifadhi takriban wakimbizi laki nne waliotoroka vurugu katika nchi hiyo yenye vikundi vingi vilivyojihami.