Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabloga na waandishi wa habari za mitandao wako mashakani: Ban

Mabloga na waandishi wa habari za mitandao wako mashakani: Ban

Ikiwa leo ni siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika salamu zake pamoja na mambo mengine ameangazia vitisho wanavyokumbana navyo mabloga na waandishi wa habari za mtandaoni.

Katika salamu zake kwenye siku hii inayotaka ustawi wa uandishi wa habari kuelekea uandishi bora, usawa wa jinsia na uslama kwenye zama za sasa za dijitali, Ban amesema vitisho dhidi ya wanahabari na mabloga hao vinatishia siyo tu haki ya msingi ya wananchi kupata habari bali pia kutoa changamoto kwa mamlaka zao.

Amesema licha ya kwamba upashaji habari kupitia mitandao kwingineko umechochea kauli za chuki, Ban amesema kwingineko kumeleta watu pamoja kwenye mijadala ya kimataifa kuhusu jinsi ya kubadilisha maisha yao yawe bora zaidi.

Ban amekumbusha kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kufanikisha ajenda ya maendeleo endelevu na hivyo ni lazima sekta hiyo iachwe ichipue kwa kuzingaita misingi ya haki za binadamu na usawa wa kijinsia wakati huu ambapo uhai wa waandishi wa habari umezidi kuwa mashakani, mwaka jana pekee 61 wakiuawa.