Mkuu wa OCHA ajionea hali ya uharibifu Nepal, asihi usaidizi Zaidi

Mkuu wa OCHA ajionea hali ya uharibifu Nepal, asihi usaidizi Zaidi

Baada ya kujionea hali halisi ya uharibifu uliosababishwa na tetemeko kubwa la ardhi nchini Nepal, Mratibu Mkuu wa masuala ya usaidizi wa kubinamu kwenye Umoja wa Mataifa amesihi jamii ya kimataifa kuimarisha usaidizi wake nchini humo.

Akizungumza mjini Kathmandu akiwa ameongoana na kamishna wa usaidizi wa kibinadamu wa Muungano wa Ulaya, EU, Christos  Stylianides, Bi. Amos amesema usaidizi huo ni muhimu kwa kuwa kiwango cha uharibifu serikali pekee haiwezi kukabiliana nao.

Ametoa shukrani kwa wito wa Waziri Mkuu wa Nepal kuhusu umuhimu wa ushirikiano katika kusaidia wahanga wa tetemeko hilo lililokumba Nepal siku saba zilizopita.

Bi. Amos ambaye pia ni Mkuu wa ofisi ya uratibu wa misaada ya Umoja wa Mataifa, OCHA ametoa hakikisho la chonbo hicho kuendeleza mshikamano na wananchi wa Nepal katika mapito ya sasa, hivyo amesema..

 (Sauti ya Bi. Amos)

 "Tunafahamu pia kwamba jambo hili linakabiliwa na changamoto ya uratibu kwa hiyo tuko hapa kujaribu kuondoa mkwamo huo, hatua inayopaswa kufanyika katika ngazi ya juu kabisa. Tuko hapa kuhakikisha tatizo hili linaonekana zaidi na linaendelea kushughulikiwa ili tupate fedha za kuweza kuendeleza jitihada za usaidizi wa kibinadamu.”

Viongozi hao wa OCHA na EU wamerejelea umuhimu wa misaada hususan maeneo ya vijijini yasiyofikika kwa urahisi wakati huu mvua za msimu wa Mansoon zikikaribia.