Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiwango cha joto duniani kipunguzwe zaidi, jukwaa lashauri UNFCCC

Kiwango cha joto duniani kipunguzwe zaidi, jukwaa lashauri UNFCCC

Mkataba wa kimataifa unaohusika na mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC umeombwa kuangalia upya uwezekano wa kupunguza zaidi kiwango cha joto duniani badala ya lengo la sasa la nyuzi joto Mbili katika kipimo cha Selsiyasi ili kunusuru sayari ya dunia na wakazi wake.

Ombi hilo limetolewa mwishoni mwa mkutano huko Ufilipino uliohusisha mataifa mataifa 20 yanayounda jukwaa la nchi zilizo hatarini kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.Mataifa hayo ni pamoja na Nepal, Ufilipino na Vanuatu ambayo hivi karibuni yamekumbwa na majanga asilia.

Katika mkutano huo ripoti tatu kutoka wataalamu na wanasayansi  zilizowasilishwa na kueleza bayana kuwa kiwango hicho cha nyuzi joto mbili hakitoshelezi na hivyo jukwaa hilo limetaka kiwango kushushwa zaidi ili kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayokiuka haki za binadamu ikiwemo watu kukosa makazi.

Ripoti hizo ziliweka bayana mathalani kiasi cha muda wa saa kazi  utakaopotea kutokana na joto kuongezeka hasa kwenye sekta ya kilimo na hivyo wamesihi angalau kiwango kisizidi nyuzi joto moja nukta tano.

Mwishoni mwa mwaka huu nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi zitakutana Paris, Ufaransa kupitisha mkataba mpya wa kudhibiti mabadiliko hayo.