Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya Haki za Binadamu yatiwa wasiwasi na ukiukaji wa haki Burundi

Ofisi ya Haki za Binadamu yatiwa wasiwasi na ukiukaji wa haki Burundi

Ofisi ya Haki za binadamu imeelezea wasiwasi wao juu ya hatua zilizochukuliwa na mamlaka za serikali ya Burundi ambazo zinazuia raia kutumia haki zao za kujieleza  na kuandamana kwa amani.

Aidha Ofisi hii imesema kuwa imeshtushwa sana na matumizi ya silaha halisia kutoka kwa na jeshi na wapelelezi wakati wa maandamano na wamezisihi mamlaka za serikali kuhakikisha kwamba viwango vya kimataifa kuhusu matumizi ya silaha kutoka kwa ofisa wa usalama vinaheshimiwa.

Halikadhalika, msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Rupert Colville, leo ameeleza kwamba mamia ya watu wamewekwa rumande tangu mwanzo wa maandamano siku ya jumapili, wakipigwa na kushikiliwa kwenye magereza yaliyojaa kupita kiasi ambapo wengine wanalazimishwa kulala wima.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Bwana Colville amesema Ofisi ya Haki za Binadamu inaziomba mamlaka za serikali kuandaa mazingira yanayotakiwa ili uchaguzi uwe huru na haki, ikiwemo kutunza haki ya kujieleza huru na kupata taarifa.