Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa juu wa OCHA na EU wako Nepal, washukuru jamii ya kimataifa

Viongozi wa juu wa OCHA na EU wako Nepal, washukuru jamii ya kimataifa

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura Valarie Amos na kamishna wa muungano wa Ulaya wa misaada ya kibinadamu na usimamizi wa migogoro Christos Stylianides, wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuwasaidia mamilioni ya watu wa Nepal walioathirika na tetemeko wakati huu wakijariibu kujenga upya maisha yao. Assumpta massoi na taarifa kamili.

(RIPOTI YA ASSUMPTA MASSOI)

Wakiwa mjini Kathmandu, viongozi hao wamesema wengi wa wahanga wa tetemeko hilo wako katika maeneo masikini na yasiyofikika .

Lakini wameshukuru juhudi zinazoendelea za serikali, mashirika ya misaada ya kitaifa na kimataifa kwa operesheni zao nchini humo.

Bi Amos ambaye baadaye atazungumza na waandishi wa habari mjini Kathmandu, amesema ameguswa sana na kutiwa moyo na ukarimu na mshikamano ulioonyeshwa hadi sasa lakini pia amesema anatambua kunahitjika msaada wa haraka wa malazi na huduma kwa waathirika, hasa wakati huu ambapo msimu wa mvua za monsoon unakaribia kwani watu wengi wamepoteza kila kitu.

Naye Bwana Stylianides amesema Muungano wa Ulaya utaendelea kutoa msaada wowote unaohitajika watakaoweza kuisaidia Nepal kurejea mtari na kusonga mbele kimaendeleo.

Wakati huo huo shirika la afya duniani linashirikiana na wadau kuepusha magonjwa ya kuhara Nepal kama anavyosema Tarik Jasarevic msemaji wa WHO.

(Sauti ya Tarik)

"Kwa sasa tunalenga kuzuia magonjwa yanayoambukizwa tukizingatia kuna suala la upatikanaji wa majisafi. Kwa sasa hatujashuhudia ongezeko la kasi la magonjwa ya kuhara lakini ni muhimu kufuatilia hali ili tuweze kuagiza mifuko ya kudhibiti kuhara kulingana na mahitaji"