Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi dhidi ya madai ya unyanyasaji wa kijinsia wa watoto CAR wafanyika: OHCHR

Uchunguzi dhidi ya madai ya unyanyasaji wa kijinsia wa watoto CAR wafanyika: OHCHR

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kuna chunguzi mbili zinazoendelea dhidi ya madai ya unyanyasaji wa kijinsia wa watoto unaodaiwa kufanywa na wanajeshi wa Kifaransa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kwa mujibu wa msemaji wa ofisi hiyo Rupert Colville , kutokana na kuendelea kwa uchunguzi huo ambao mmoja unafanywa na serikali ya Ufaransa ofisi ya haki za binadamu inajizuia kuhusu nini cha kusema zaidi katika wakati huu.

Hata hivyo ameongeza kuwa uchunguzi huu ni muhimu saana hasa kutokana na unyeti wa madai yenyewe

(SAUTI YA RUPERT COLVILLE)

“ Madai ya nini kilichotokea kwa watoto hawa hayafikiriki. Maelezo yaliyomo katika mahojiano na waathirika na mashahidi yaliyofanywa na wapelelezi wa Umoja wa Mataifa mwaka jana , ikiwa ni pamoja na mfanyakazi wetu ni machukizo kabisa. Tunashukuru kwamba mamlaka ya Ufaransa wanachunguza hili na wamesema wanapanga kutoa wito wa adhabu kali chini ya sheria kwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia.”