Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vurugu Burundi zakiuka misingi ya demokrasia: Watalaam UM

Vurugu Burundi zakiuka misingi ya demokrasia: Watalaam UM

Kundi la wataalam wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu wamelaani leo ghasia inayoendelea nchini Burundi na wamezisihi mamlaka za serikali kukuza haki za binadamu, zikiwemo haki ya kujieleza na haki ya kuandamana kwa amani.

Katika taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa, wataalam hao wametoa wito kwa uchunguzi huru kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu uliofanyika kwa kipindi cha siku chache zilizopita, ambapo wanaharakati wa haki za binadamu wamelengwa, vyombo vya habari kufungwa, na silaha za ukweli kutumika dhidi ya waandamanaji.

Aidha wametoa onyo kuhusu vitendo vinavyofanywa na kundi la vijana wanamgambo wa Imbonerakure, na kusikitishwa kwamba vijana hawa wanakubaliwa na chama tawala. Wataalam wa Umoja wa Mataifa wameiomba serikali isalimishe mara moja wanamgambo hawa.

Miongoni mwa wataalam walioshirikiana katika kutoa wito huo ni Maina Kiai kutoka Kenya ambaye ni mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kuandamana kwa amani.

Hatimaye wataalam hao wamesema vurugu hizo zinaweza kuharibu mafanikio yote yaliyopatikana nchini humo baada ya makubaliano ya Arusha ya mwaka 2000 na kuridhiwa kwa katiba mpya mwaka 2005, iliyoweka rasmi ugawaji wa uongozi baina ya makabila ya Burundi na kukuza hali ya maridhiano nchini humo.