Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola: Benki ya Dunia, FAO yasaidia serikali Guinea kukwamua wananchi

Ebola: Benki ya Dunia, FAO yasaidia serikali Guinea kukwamua wananchi

Hatimaye serikali ya Guinea kwa ushirikiano na Benki ya dunia na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO wamefanikiwa kuanzisha miradi yenye lengo la kukwamua uzalishaji wa kilimo kwa kaya zilizoathirika na Ebola.

Taarifa ya FAO imesema mradi huo wa pamoja unalenga kupunguza madhara Ebola kwenye sekta hiyo miongoni mwa wananchi ambapo utasaidia kuboresha lishe kwenye mji mkuu Conakry na mikoa ya Gueckedou, Macenta, Kissidougou, Kouroussa Siguiri N'Nzérékoré, Forécariah Kérouané Coyah, Beyla na Kindia.

Kupitia mradi huo jumla ya kaya 18 660 zitapatiwa mbegu za mahindi, mpunga, mboga za majani pamoja na pembejeo kama vile mbolea kwa ajili ya msimu ujao wa upanzi.

Matarajio ni kuzalisha tani 9,000 za mpunga na 4,800 za mahindi ambapo wakulima wataweza kupata chakula na kipato kutoka mauzo ya baadhi ya mavuno yatatumika kugharimia elimu na afya.

Benki ya dunia imachangia dola Milioni Tano zikigharimia kampeni za uhamasishaji kaya 30,000 ili kukinga kuenea kwa Ebola maeneo ya vijijini.