Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa mafuta wasitisha mgao wa chakula Yemen: WFP

Uhaba wa mafuta wasitisha mgao wa chakula Yemen: WFP

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limelazimika kusitisha mgao wa chakula kwa wahitaji kwenye baadhi ya maeneo nchini Yemen kutokana na kuishiwa mafuta.

Mwakilishi wa WPF nchini humo Purnima Kashyap amesema uhaba wa mafuta mapema wiki hii umesababisha washindwe kusambaza chakula magharibi mwa jimbo la Hudyda, na hali inavyoendelea tatizo hilo litakuwa kubwa zaidi.

Amesema wanahitaji zaidi ya lita Laki Mbili za mafuta ili kuendelea kusambaza misaada ya chaukla ambacho tayari kiko kwenye ghala lake, chakula ambacho kinatosha kulisha watu Milioni Moja nukta Nne kwa mwezi mmoja.

Bi. Kashyap amesihi pande husika katika mzozo wa Yemen kuruhusu wafanyabiashara na mashirika ya misaada kupeleka mafuta yanayohitajika ili kusambaza shehena za misaada.

Katika wiki mbili zilizopita, WFP imefikisha mgao wa dharura wa chakula kwa watu Laki saba katika majimbo ya Aden, Sana’a, Hajjah, Hudayda, Amran, Al Mahwit na Dhamar.