Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mitandao ya kijamii Burundi yafungiwa: OCHA

Mitandao ya kijamii Burundi yafungiwa: OCHA

Nchini Burundi , maandamano yameendelea leo siku ya tano kwenye vitongoji vitano vya mji mkuu Bujumbura, ambavyo ni Mutakura, Cibitoke, Kanyosha, Bwiza na Musaga na hadi sasa kusababisha vifo saba wakiwemo polisi wawili.

Kwenye maeneo mengine ripoti zinasema hali imetulia kiasi, hata hivyo shule na maduka bado vimefungwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa maziwa makuu Said Djinnit bado anazungumza na viongozi nchini humo ili kupata suluhu kwa mzozo huo.

Aidha taarifa iliyotolewa leo na OCHA inasema mitandao ya kijamii ya Twitter, Facebook, Viber na WhatsApp imefungwa, halikadhalika redio moja, wadau kutoka kwa mashirika ya kibinadamu wakionya kwamba uamuzi huo unaweza kuchochea wasiwasi zaidi katika jamii.

Wakati huo huo, mpango wa mashirika ya kibinadamu kwa uchaguzi wa Burundi umetangazwa jumatano hii mjini Nairobi, ukitaja mahitaji ya ufadhili wa dola milioni 11 kwa ajili ya watu 50,000 hadi 350,000 ambao wataweza kuathirika baada ya uchaguzi iwapo vurugu itatokea.