Dola Milioni Nane zahitajika kukwamua wakulima Nepal:FAO
Wakati mkuu wa masuala ya usaidizi wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Valerie Amos akielekea Nepal kuangalia hali halisi baada ya tetemeko la ardhi kukumba nchi hiyo, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema dola Milioni Nane zahitajika haraka ili kunasua wakulima nchini ambao shughuli zao za kilimo zimekwama kufuatia tetemeko hilo.
FAO inasema msaada huo ni muhimu kuwezesha wakulima kupata pembejeo za kilimo ili warejee kwenye shughuli zao maandalizi ya upanzi wa mpunga kwa kuwa msimu ndio sasa.
Kwa mujibu wa FAO wakulima wakishindwa kufanya hivyo sasa watakosa mavuno ya mpunga ambao ni zao tegemewa la chakula nchini Nepal na hivyo uhakika wa chakula utakuwa mashakani.
Somsak Pipoppinyo ni mwakilishi wa FAO huko Nepal na Bhutan.
(Sauti ya Somsak)
"Ili kurejesha maisha yao ya zamani, kwa sasa hivi waathiriwa wanalenga namna ya kupata nyumba, maji safi, na mazingira safi, lakini tunahitaji kuanza maandalizi ya baadaye, tunashirikiana kwa karibu na wizara ya kilimo kutambua matatizo yaliyopo, kwani kilimo ndio msingi wa maisha na uchumi wa nchi hii. "