Australia kumkatalia visa raia wa Iran kwa sababu za usalama ni ukiukaji wa haki za familia:UM

Australia kumkatalia visa raia wa Iran kwa sababu za usalama ni ukiukaji wa haki za familia:UM

Australia imekiuka haki za maisha ya familia dhidi ya raia wa Iran aliyelazimika kuondoka nchini humo baada ya miaka 16 kwa sababu anachukuliwa kama tishio kwa usalama wa taifa , lakini hakuwahi kuambiwa ni kwanini , imebaini kamati ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu.

Raia huyo wa Iran Mansour Leghaei alinyimwa kibali cha kukaa moja kwa moja nchini Australia kutokana na kile serikali inachosema ni sababu nzito za usalama wa taifa.  Ingawa ndugu wa familia yake wana haki ya kusalia Australia , mke wa Bwana Leghaei na binti yake aliyezaliwa Australia aliyekuwa na miaka 14 wakati huo, waliondoka kwenda Iran pamoja naye Juni 2010.

Watoto wake mapacha wa kiume raia wa Australia waliokuwa na umri wa miaka 26 wakati huo na mwanaye mwingine wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 20 wakati huo walisalia Australia.

Kamati ya haki za binadamu mjini Geneva imesema kitendo cha Australia kumnyima visa kilichosababisha familia kuchagua ama kuambatana na bwana Leghaei au kusalia Australia kimeingilia haki ya bwana Lehaei ya kuwa na maisha ya familia.

Kamati imesema bwana Leghaei ameishi Australia kwa miaka 16 kihalali, bila kuwahi kushitakiwa au kuonywa kwa kosa lolote na mamlaka za sheria za Australia, hivyo kamati imeona kwamba Australia imekiuka kifungu namba 17 na 23 cha agano la kimataifa la haki za kiraia na kisiasa.

Kwa upande wake Australia imedai kwamba uamuzi wake wa kumfukuza bwana Leghaei ulifikiwa na sheria za Australia ambazo zinazingatia agano hilo.