Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mliotoa ahadi kwa mtaji wa GCF timizeni ahadi kabla ya 30 Aprili. Ban

Mliotoa ahadi kwa mtaji wa GCF timizeni ahadi kabla ya 30 Aprili. Ban

Akiwa ziarani nchini Ufaransa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezikumbusha nchi zilizoahidi kuchangia mtaji wa jumla ya dola Bilioni 10 za mfuko wa mabadiliko ya tabianchi, GCF,  kufanya hivyo mapema kabla ya tarehe ya mwisho ya kuwasilisha fedha hizo ambayo ni 30 mwezi huu wa Aprili.

Ban amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Paris baada ya mazungumzo yake na Rais Francois Hollande wa Ufaransa, mkutano ambao rais huyo pia alihudhuria.

Katibu Mkuu ameshukuru Ufaransa kwa kutimiza mchango wake huku akisema kukamilisha ahadi yake kwa GCF ni muhimu ili kufadhili miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wakati dunia inatarajia kupitisha mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi baadaye mwaka huu mjini Paris.

Halikadhalika Ban amegusia ghasia zinazoendelea duniani, akisema katika mkutano wa 70 wa Umoja wa Mataifa amepanga kuwasilisha mpango wa kukabiliana na misimamo mikali inayoibua mizozo.