Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kobler aamini ushirikiano baina ya MONUSCO na FARDC utaanza tena hivi karibuni

Kobler aamini ushirikiano baina ya MONUSCO na FARDC utaanza tena hivi karibuni

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, hauna orodha ya wanajeshi wa serikali waliojihusisha na ukiukaji wa haki za binadamu, amesema mkuu wa MONUSCO Martin Kobler, akitambua kazi muhimu inayotekelezwa na jeshi hilo la kitaifa.

Amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa, na kuongeza kwamba MONUSCO imeipatia serikali ya DRC masharti ambayo jeshi la FARDC linapaswa kufuatilia iwapo litataka kuongeza kushirikiana na mpango huo.

Bwana Kobler amesema masharti hayo siyo magumu na anaamini kwamba tatizo hilo litatatuliwa bila kuchelewa kwani ushirikiano baina ya MONUSCO na FARDC ni muhimu sana

“ Tuna maeneo ambayo yanatawaliwa na vikundi vilivyojihami, kwa sasa hasa FDLR. Karibu kila wiki naenda kwenye maeneo hayo, Nyamilima, Kihoto, Nyanzulu, na maeneo mengine. Najua kwamba watu wanateseka. Najua kwamba watu wanasubiri tuanzishe upya ushirikiano hapa”

Mkuu wa MONUSCO amesema swala hilo lilikuwa miongoni mwa mada zilizozungumzwa wakati wa ziara ya mkuu wa idara ya operesheni za kulinda amani ya Umoja wa Mataifa, DPKO, Hervé Ladsous nchini humo iliyofanyika siku chache zilizopita.

Aidha Bwana Kobler amewaambia waandishi wa habari kwamba Mkuu wa DPKO amekuwa na mazungumzo na rais Joseph Kabila na viongozi wa kisiasa na kijamii. Pia Bwana Ladsous amehudhuria hafla ya kuwaaga walinda amani 850 mjini Bukavu ikiwa ni moja ya hatua za mkakati wa kuondoka kwa MONUSCO nchini DRC